Kutuhusu

TUNAYOFANYA

TUNAYOFANYA
Avaaz ni mwandani, na kimbilio, kwa wanyonge kila mahali.

Zainab Bangura
Mkurugenzi Mkuu katika UNON
Avaaz — ikimaanisha “sauti” katika lugha kadhaa za Ulaya, Mashariki ya Kati na Asia— ilizinduliwa mwaka wa 2007 kwa dhamira rahisi ya kidemokrasia: kuwaleta raia wa mataifa yote pamoja ili kuziba pengo kati ya ulimwengu tulionao na ulimwengu ambao watu wengi kila mahali wanataka.

Avaaz huwawezesha mamilioni ya watu wa asili mbalimbali kuchukua hatua katika masuala ya kimataifa, kikanda na kitaifa, kutoka kwa ufisadi na umaskini hadi migogoro na mabadiliko ya hali ya anga. Mtindo wetu wa uandalizi wa kimtandao hufanya maelfu ya juhudi za watu binafsi, hata ziwe ndogo kiasi gani, kuunganishwa kwa haraka na kuwa nguvu madhubuti ya pamoja. (Soma kuhusu matokeo kwenye ukurasa wa Vidokezo.)

Jamii ya Avaaz hufanya kampeni katika lugha 15, zinazohudumiwa na timu kuu katika mabara 6 na maelfu ya watu waliojitolea. Pamoja tunachukua hatua -- kutia kampeni saini, kufadhili kampeni za vyombo vya habari na hatua za moja kwa moja, kutuma baruapepe, kuzipigia simu na kuzishawishi serikali, na kuandaa maandamano na matukio halisi -- ili kuhakikisha kuwa maoni na maadili ya raia duniani yanaarifu maamuzi yanayotuathiri sisi sote.

Mtindo wa Avaaz: Jinsi Tunavyofanya Kazi

Kutokana na teknolojia, umahiri na wepesi wa kufanya harakati

Makundi na mashirika ya kimataifa ya raia na ya kijamii ya awali yamelazimika kuandaa harakati tofauti kwa kila suala linaloibuka, mwaka hadi mwaka na nchi baada ya nchi, ili kufikia kiwango ambacho kinaweza kuleta mabadiliko.

Hii leo, kutokana na teknolojia mpya na kuibuka kwa maadili ya kutegemeana kimataifa, hicho si kikwazo tena. Huku mashirika mengine ya kiraia ya kimataifa yakiwa yameundwa na vikundi mbalimbali vya kitaifa vinayoangazia masuala tofauti, kila kimoja kikiwa na wafanyakazi, bajeti, na muundo wa kufanya maamuzi binafsi, Avaaz ina timu moja ya kimataifa yenye mamlaka ya kushughulikia suala lolote linalohusu umma- - jambo linalosababisha kampeni zake kuwa zenye unyumbufu wa ajabu, umakini na za kiwango kikuu.

Jumuiya ya mtandaoni ya Avaaz inaweza kuwa kama kipazasauti ili kuelekeza makini ya watu kwenye masuala mapya; mhunzi anayeyachukua yale wanayoyajali raia na kuyatia katika kampeni maalum; gari la wazima-moto linalowasilisha msaada mwafaka kwa jambo la ghafla na dharura; na kiungo cha seli kinachokua na kuchukua umbo lolote lile la utetezi au kazi yoyote ile inayofaa zaidi kukidhi haja ya dharura.

Vipaumbele na nguvu za Avaaz hutoka kwa wanajumuiya

Kila mwaka, Avaaz huviweka vipaumbele vya jumla kupitia kura za wanajumuiya pekee. Mawazo ya kampeni huchagizwa na kujaribiwa kila juma kupitia sampuli nasibu ya wanajumuiya 10,000—na ni mipango inayoungwa mkono kwa asilimia kuu pekee inayopelekwa katika kiwango cha juu. Baada ya hapo, kampeni zinazowafikia wanajumuiya wote hufanywa maarufu zaidi na, aghalabu, mamia ya maelfu ya wanaAvaaz wanaochukua hatua katika siku au hata saa chache.

Maadili ya uongozi-utumishi

Wafanyakazi wa Avaaz huandika arifa za baruapepe kwa jumuiya ya Avaaz jinsi msaidizi wa kibinafsi anavyompasha habari rais au waziri mkuu: tuna muda mfupi tu wa kuwasilisha maelezo muhimu ambayo msomaji anahitaji ili kuamua ikiwa atahusika, na kampeni inategemea uamuzi huo.

Ili kuhakikisha kuwa hatupotezi wakati wowote wa wasomaji wetu, ni kazi ya wafanyakazi wetu kutafuta jinsi ya kuzifanya dakika hizo chache, zikizidishwa kwa idadi kubwa ya watu, zinaweza kuleta mabadiliko ya kweli kwenye suala muhimu. Wafanyakazi hushirikiana na wadau na wataalamu mbalimbali ili kuendeleza mikakati ya kampeni yenye ufanisi, inayoendeshwa na wanajumuiya; kuifanya mihtasari kupitia arifa zilizo wazi na zenye mvuto; na, ikiwa wanaAvaaz wataamua kuchukua hatua zaidi ya hapo, huhakikisha kwamba kampeni inatekelezwa kupitia—kuwasilisha maombi na jumbe za wanajumuiya, kuandaa kampeni za matangazo zilizofadhiliwa na wanajumuiya, au chochote kingine kile kinachohitajika.

Hii ni kusema kuwa, wafanyakazi wa Avaaz hawaweki ajenda kisha kujaribu kuwashawishi wanajumuiya kukubaliana nayo. Hali halisi inakaribia kinyume chake: wafanyakazi huwasikiliza wanajumuiya na kupendekeza hatua wanazoweza kuchukua ili kuleta mabadiliko ulimwenguni. Si ajabu, basi, kwamba kampeni zetu nyingi zinazopata kufanikiwa zaidi hupendekezwa kwanza na wanajumuiya wa Avaaz wenyewe. Na uongozi ni sehemu muhimu ya huduma yetu kwa wanajumuiya: panahitajika maono na ujuzi kutafuta na kuwasiliana njia ya kuunda ulimwengu bora.

Tunazingatia fursa za mabadiliko zinazojitokeza wakati wa dhiki

Suala linapoibuka na kukua, hutokea wakati fulani ambapo uamuzi lazima ufanywe, na mwito mkuu wa raia unaweza kuyabadili mambo kwa ghafla. Kufikia hatua hii kunaweza kuchukua miaka mingi ya kazi ya sulubu, kazi ambayo kwa kawaida huwa ni sawa na msingi wa nyumba usioonekana lakini ni muhimu kupindukia, na inatekelezwa na watu waliojitolea vilivyo kiasi cha kutozingatia chochote kingine. Lakini wakati mwafaka unapowadia, na mwanga wa makini ya umma unapoliangazia suala, maamuzi muhimu huchukua mkondo mmoja au mwingine kulingana na mtazamo wa viongozi kuhusu athari za kisiasa za kila chaguo. Ni katika fursa hizi za kipekee wakati wa dhiki ambapo jumuiya ya Avaaz aghalabu hujitokeza na kufanya mabadiliko.

Katika nchi au suala fulani, fursa hizo huenda zikapatikana mara moja au mbili tu kwa mwaka. Lakini kwa vile Avaaz inaweza kufanya kazi katika nchi zote na kuzingatia masuala yote, fursa hizi zinaweza kuchipuka mara kadhaa kwa juma.

Muundo wetu wa kufadhiliwa na wanajumuiya hutuweka huru na kutufanya kuwajibika

Kwa sababu Avaaz inafadhiliwa na wanajumuiya kikamilifu, uwajibikaji wa kidemokrasia umejikita katika moyo wetu. Hakuna mfadhili wa shirika la kibinafsi au mkuu wa serikali anayeweza kuishurutisha Avaaz ibadilishe vipaumbele vyake ili kuwiana na ajenda fulani za nje—katu hatukubali fedha kutoka kwa serikali au mashirika ya kibinafsi. (Soma zaidi kuhusu kwa nini kuchangia Avaaz ni jambo bora na la manufaa hapa, na utoe mchango hapa.)

Badala ya kugawanyika na kutawanyika, tunakusanyika na kukua—tukiunganishwa na maadili

Harakati, miungano, na mashirika mara nyingi huvunjika katika vipande vingi vidogo kadri muda unavyosonga —au hujipata yakitumia zaidi na zaidi ya muda wao yakijaribu kuyatangamanisha makundi yanayozozana. Hapa Avaaz, tunatambua kwamba watu wenye nia njema mara nyingi watatofautiana katika mambo maalum; badala ya kukazania sote tulikubali jambo fulani, kila mmoja wetu hujiamulia mwenyewe ikiwa atashiriki katika kampeni fulani.

Lakini msingi wa kampeni za Avaaz ni fungu la maadili - imani kwamba kabla ya mengine yote sisi sote ni binadamu, na tumetunukiwa wajibu kila mmoja kwa mwingine, kwa vizazi vijavyo, na kwa dunia yetu. Masuala tunayoyafanyia kazi ni vielelezo maalum vya maadili hayo. Hivyo basi, tena na tena, Avaaz hushuhudia jambo lile lile: kwamba watu wanaojiunga na jumuiya yetu kupitia kampeni inayoangazia suala moja huchukua hatua kwenye suala jingine, na kisha jingine. Hii ni chanzo ya matumaini makubwa: kwamba ndoto zetu zinawiana, na kwamba, kwa pamoja, tunaweza kujenga daraja itakayotuvusha kutoka kwa ulimwengu tulionao sasa hadi kwenye ulimwengu ambao sote tunautamani.

Kampeni nyingi za Avaaz huanzishwa na wanajumuiya wetu. Ni rahisi - bofya ili kuanzisha yako sasa na kushinda katika suala lolote lile - liwe la kikata, kitaifa au kimataifa.